Hivi karibuni kumejitokeza mkanganyiko mkubwa kati ya wamiliki wa vyombo vya habari, hususan vya luninga, na Serikali, kuhusu kile kinachoaminika kuwa kutokujipanga vizuri kwa Serikali katika zoezi zima la kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda mfumo wa digiti, kwa upande wa luninga.
Hali hii imejidhihirisha kutokana na ukweli kwamba, licha ya kwamba gharama za vifaa ambavyo vinahitajika kukamilisha zoezi hilo ni kubwa sana (hususan kwa kuwa bei za soko bado hazijaimarika na Serikali haijaamua kufuta kodi kwenye vifaa hivyo), lakini kwa upande mwingine, wataalam wenye dhamana ya kutoa ushauri kuhusu ufanisi mzuri wa zoezi hili wameamua kuugeuza mchakato huu kuwa mradi mkubwa wa kujipatia fedha nyingi, kwa kuwa tu wameweka usiri mkubwa kwenye mfumo mzima, na wale wanaotoa ushauri huo wanautoa kwa gharama kubwa sana.
Kinachokera zaidi si tu kwamba inaonekana dhahiri kwamba usiri huu kati ya wataalam wa dijiti na Serikali ulipangwa tangu awali, lakini kibaya zaidi ni kwamba, Serikali imeamua kufuta tu kodi ya VAT kwenye visambuzi pekee, jambo ambalo halijasaidia kwa kuwa gharama za mitambo, ile inayomilikiwa na wenye leseni za kurusha matangazo ya dijiti, yaani, Multiplex Operators (MUX) kama vile StarMedia (Star Times), ZUKU TV, DSTv, EasyTV, ATN, n.k., na wamiliki wa vituo vya luninga, yaani wenye leseni za Content Service Provider (CSP), ni kubwa kiasi kwamba inakuwa si rahisi kwa wamiliki hawa kuweza kuzimudu kwa wakati mmoja, haswa ikizingatiwa kwamba Serikali bado haijafuta kodi kwenye vifaa hivyo. Ughali wa vifaa hivi, kwa upande wa MUX na CSP, unasababisha, hatimaye, gharama ya visambuzi kwa watumiaji wa mwisho, ambao nao wanatakiwa kulipia gharama za kila mwezi, bado kuwa kubwa.
Kizungumkuti hiki kinatokana na mfumo mzima ambao umeundwa na Serikali, ambao, awali ulionekana kuwa mzuri, lakini sasa unaonekana kuwa mbovu kupita kiasi.
Serikali, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilianzisha mfumo wa Leseni Jumuishi (Convergence Licensing Framework), ambapo kampuni iliweza kulipia leseni moja na kuruhusiwa kufanya shughuli nyingi kwa wakati mmoja. Hata hivyo, leseni za Multiplex Operators bado ziliendelea kutolewa peke yake, tofauti na CLF, jambo ambalo limezua mkanganyiko.
Kana kwamba hilo halitoshi, Serikali bado ikazua leseni nyingine mbili, yaani, Content Producer na Content Service Provider, yaani, Mtayarishaji wa Maudhui na Mtoa Huduma ya Maudhui, ambaye kwa kawaida huwa mwenye kituo cha luninga au redio. Kwenye mfumo uliowekwa hivi sasa, haiyumkini Content Producer akawa tofauti na mwenye kituo cha luninga au redio, kwani, vituo vyote vya luninga na redio hapa nchini na kama ilivyo nchi zote hutayarisha vipindi (maudhui) vyao na kuvirusha kwa watazamaji. Kwa hiyo, Content Producer (CP), kwa mtazamo wa luninga na redio, hapa anakuwa sawa na Content Service Provider (CSP).
Sasa tumtazame huyu CSP. Ni mambo gani yanayomsibu?
Kwanza kabisa, ili aweze kurusha matangazo yake hadi kumfikia mtazamaji ambaye anamiliki kisambuzi, anapaswa kununua vifaa ambavyo vitamwezesha kusafirisha matangazo (signal) yake kwenda kwa Multiplex Operator (MUX); vifaa ambavyo vina gharama kubwa na ambavyo upatikanaji wake unafanywa kuwa SIRI kubwa. Hili ni fungu la kwanza la gharama. Pili, ili matangazo hayo yaweze kufika kwa MUX, lazima apatikane mtu wa kuyasafirisha, haswa kwa watangazaji wa mikoani. MUX wengi bado hawajaweka vifaa vinavyowawezesha CSP kujiunga nao moja kwa moja, yaani, Point of Presence (PoP), kwa hiyo inawalazimu CSP kupitia kwa kampuni za mawasiliano, kama vile TTCL, ili kuweza kulipia njia za kusafirishia matangazo hayo. Hili ni fungu la pili la gharama, ambao, iwapo MUX wangekuwa wameweka PoPs za kutosha mikoani, kusingekuwa na gharama za kusafirishia matangazo (broadband data transmission) kwani CSP wangetumia vifaa vya kusafirisha matangazo kwa kutumia mawimbi ya redio (digital data transmission), jambo ambalo lingeondoa uwepo wa gharama za kusafirisha matangazo kwa njia ya broadband data transmission. Kana kwamba gharama hizi hazitoshi, kwa mujibu wa maelezo kutoka TCRA, MUX nao wanawatoza CSP gharama za kurusha channel au idhaa moja kwa mwezi kuwa wastani wa Dola za Marekani 3,800/=, kiasi ambacho ni kikubwa na wamiliki wengi wa vituo vya luninga hawawezi kukimudu kwa urahisi. Utata mwingine ni pale ambapo TCRA wamependekeza kiwango hiki kikubwa bila kufafanua namna ambavyo kimefikiwa, jambo ambalo limewakwaza wamiliki wengi wa vituo vya luninga, hususan waliopo mikoani.
Jambo ambalo binafsi ninajiuliza ni, je, Serikali ilikuwa na nia dhahiri ya kuwawezesha wamiliki wa vituo vya luninga (CSP) kuhamia kikamilifu kwenye mfumo wa dijiti, kwani inaonekana wazi kwamba, Serikali haikujipanga na ilikurupuka tu kufanya zoezi hili, haiyumkini kwa sababu gani. Iwapo Serikali ingekuwa na nia ya kuwawezesha CSP kukamilisha zoezi hili, kwanza kabisa ingefuta kodi zote kwenye vifaa vyote vinavyohitajika kwenye mfumo mzima wa dijiti, kwa kuwa vifaa hivyo ni ghali. Pili, Serikali ingefuta kodi zote kwenye gharama za kurusha matangazo kwa njia ya mitandao (ama ya simu au ya mawasiliano tarakinishi) ili kuwezesha CSP wengi zaidi kumudu gharama hizo. Tatu, Serikali ingepunguza kiwango cha malipo ya mwezi ya gharama za kurusha idhaa moja, na gharama hizo zitozwe kwa Shilingi ya Kitanzania badala ya Dola za Kimarekani.
Hii ingesababisha, si tu kwamba gharama za visambuzi kuwa nafuu, lakini pia, wamiliki wengi wa luninga kuweza kuhamia kikamilifu kwenye mfumo huu wa dijiti, hatimaye nchi nzima kufanikiwa kikamilifu.
Kwa hali iliyopo sasa, mkanganyiko huu hautaleta tija kwa yeyote, maslahi ya taifa hayatazingatiwa, atakayeumia ni CSP na mteja wa mwisho, mtazamaji. Lakini pia, watakaokwazika zaidi ni watangazaji wa biashara; watatangaza nini ilhali vituo vya luninga havionekani kwa watazamaji?
Serikali ijipange upya. Iache ubishi katika suala hili.